11 Aprili 2025 - 18:41
Source: Parstoday
Waliofariki dunia klabuni Jamhuri ya Dominika wafikia 218

Maafisa wa serikali katika Jamhuri ya Dominika wamesema idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mkasa wa kuporomoka kwa paa katika ukumbi wa starehe wa Jet Set katika mji mkuu Santo Domingo imepindukia 200, huku matumaini ya kupata manusura yazidi kukififia.

Vyombo vya habari nchini humo vimemnukuu Mkurugenzi wa Operesheni za Dharura nchini humo, Juan Manuel Mendez, akisema jana Alkhamisi kwamba, takriban watu 218 wamefariki dunia katika ajali hiyo, na wengine 189 "wameokolewa wakiwa hai". Mendez amesisitiza kuwa idadi hiyo ni "takwimu ya awali" na kwamba kuna uwezekano wa idadi hiyo kuongezeka.

Mendez ameuambia mkutano wa wanahabari kuwa, "Hatutamtelekeza mtu yeyote mpaka tutakapomaliza kila kitu. Tutakuwa hapa hadi tutakampopata kila mtu, aliyekufa au aliye hai," na kuongeza kuwa, hakuna manusura aliyepatikana chini ya vifusi tangu Jumanne mchana.

Klabu hiyo ya usiku ilikuwa imejaa wanamuziki, wanamichezo mashuhuri na maafisa wa serikali wakati vumbi lilipoanza kudondoka kutoka kwenye dari na kwenye vinywaji vya watu mapema Jumanne. Dakika chache baadaye, paa lilianguka na kusababisha maafa makubwa.

Habari zaidi zinasema kuwa, idadi kubwa ya marafiki na jamaa wameendelea kukusanyika nje ya Taasisi ya Kitaifa ya Uchunguzi wa Kipatholojia ya Jamuhuri ya Dominika, wakisubiri habari zozote kuhusu hatima za wapendwa wao.

Si vibaya kuashiria hapa kuwa, mwezi uliopita, moto uliokumba klabu ya anasa katika mji wa Kocani, Macedonia Kaskazini usiku wa manane wa kuamkia leo ulisababisha makumi ya watu kuaga dunia na kujeruhiwa.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha